“BAADA ya muziki wetu wa
vijana kukataliwa kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini,
niliona njia pekee ni kuanzisha kituo cha redio ya burudani ili kutangaza
kazi na vipaji vya vijana.”
Hiyo ni kauli ya Joseph Alex Kusaga 'Joe’, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni
ya Clouds Media Group inayomiliki vituo vitatu vya redio vya Clouds FM,
Choice FM, Coconut FM, na kituo cha televisheni cha Clouds.
Pia anamiliki makampuni tanzu kadhaa. Kwa ujumla, Kusaga si tu kwamba
amefanikiwa kisanii, bali amefanikiwa pia kimaisha kiasi cha kuwa mmoja
wa vijana wa kupigiwa mfano nchini.
Hata hivyo, katika mazungumzo na HABARILEO Jumapili, Kusaga anakiri
safari yake ya kuyafikia mafanikio aliyonayo haikuwa rahisi hata kidogo.
Alianzia mbali, akiwa mchezeshaji disko, yaani DJ tangu akiwa mwanafunzi
wa Sekondari ya Mzizima, jijini Dar es Salaam mwaka 1985.
“Kupuuzwa kwa muziki wa vijana ndiko kulikochangia kuwa na wazo la
kuanzisha kituo cha redio,” anasema Kusaga, miongoni mwa wasanii
wanaojishughulisha na muziki wa kisasa tangu miaka ya 1980 na 1990,
lakini huku nyimbo zao zikipingwa kwa kile kilichokuwa kinaaminika kuwa
ni muziki wa kihuni.
Kusaga, ambaye wakati huo alikuwa kama kamanda wa muziki wa kizazi kipya
alikwazika kwa kuwa hakukuwa na njia rahisi ya kutangaza muziki wa vijana
bila kupitia kwenye redio.
Hata hivyo hakukata tamaa, aliamua kuweka mikakati ya kuanzisha redio ya
burudani kwa lengo la kuwapatia vijana fursa ya kutangaza kazi na vipaji
vyao bila vikwazo.
Tofauti na wasanii wenye tabia ya kufuja mali kwa lengo la kujipatia
umaarufu, Kusaga alizingatia usemi wa wahenga kuwa `Fahari ni Mama wa
Ujinga’. Hivyo alidunduliza fedha zake kwa lengo la kukusanya mtaji wa
kuanzisha redio.
Anasema kwamba, ingawa kila alipozungumzia suala la kuanzisha redio, watu
wengi walitilia shaka uwezo wake hakukata tamaa kwa kuwa aliamini anaweza
kutimiza ndoto yake ya kumiliki redio kwa ajili ya sauti za wanyonge.
Ili kutimiza lengo hilo Kusaga aliandaa matamasha mbalimbali kwa lengo la
kuwajumuisha wanamuziki chipukizi kutoa burudani kwa mashabiki wa muziki
wa kizazi.
“Niliendelea kuandaa matamasha huku nikifanya utafiti wa kuanzisha
redio…baada ya mtaji wangu kuongezeka niliomba mkopo benki niweze
kufanikisha azma yangu,” anaeleza. Hata hivyo haikuwa rahisi kupata mkopo
ila hakukata tamaa.
Alivuta subira na kuendelea kuhangaika hadi alipofanikiwa kupata mkopo
huo. Pia alianzisha club za burudani katika hoteli mbalimbali kwa lengo
la kutunisha mtaji wake.
“Pia nilipata changamoto kidogo wakati wa kuomba leseni ya kufungua kituo
cha redio…walitilia shaka umri wetu, lakini waliamua kutupatia kwa kuwa
tulifaulu kujibu maswali na kutimiza masharti yote.
Baada ya kupata leseni Kusaga na timu yake walikaa mwaka mzima kabla ya
kufanikisha lengo lao.
“Baada ya kupata leseni niliamua kujikita katika utafiti wa kina na
kutafuta njia ya kuhimili ushindani wa muda mrefu kwa kuzingatia matumizi
ya teknolojia ya kisasa na mahitaji ya Watanzania,” anaeleza.
Katika utafiti wake alibaini kuwa asilimia kubwa ya magari yaliyopo
Tanzania ni ya Kijapani na yana redio ambazo hazina uwezo wa kukamata
stesheni mbalimbali za redio.
Hivyo alitumia mbinu kuhakikisha kuwa kituo chake cha Clouds kinasikika
katika magari jambo ambalo lilimuwezesha kuvuma kwa haraka.
“Wakati redio Clouds ilipoanzishwa mwaka 1998 iliweza kusikika katika
magari yote yaliyopo Dar es Salaam hivyo ilikuwa rahisi kufahamika,”
anaeleza.
Hivyo ndivyo ilivyozaliwa Clouds FM yenye kauli mbiu 'Redio ya Watu’,
hivyo kutimiza ndoto ya muda mrefu ya Kusaga aliyoianza wakati anaanzisha
disko lake katika ukumbi wa Hellenic jijini Dar es Salaam mwaka 1985.
Miaka miwili baadaye, baada ya kupata ujasiri zaidi alianzisha disko
lililoitwa Clouds, wakati huo yeye mwenyewe akiwa mchezeshaji, yaani DJ,
akitumia jina la DJ Emperor.
Hakuna shaka kwamba, disko la Clouds lilitia fora na kuliteka Jiji tangu
lilipokuwa linaporomoshwa katika kumbi za Motel Agip `Shimoni’, New
Africa, Twiga House, Kilimanjaro Hotel (Pool side) na Hotel Seventy Seven
mjini Arusha kabla ya baadaye kuanzisha klabu yake iliyoitwa Mawingu Club
huko Arusha.
Ni disko la Clouds ndilo lililotamba pia katika kumbi kama TAZARA pale
Kinondoni na kumbi nyingine za ndani na nje ya Dar es Salaam.
Mambo yalikwenda yakiongezeka na kufikia mwaka 2000, alianzisha studio
yake ya kisasa iliyoitwa Mawingu Studio eneo la Mwenge, Dar es Salaam.
“Mitambo hiyo imesaidia kurekodi nyimbo sanjari na matumizi ya kisasa ya
mitambo ya kisasa ya kurushia matangazo. Pia Studio hiyo inapunguza
vikwazo vya vijana ambao wanaimba nyimbo nzuri, lakini wanakosa sehemu ya
kurekodia,” anasema.
Ujio wa studio hiyo ulikuja miaka miwili tangu kuanzishwa kwa kituo cha
redio cha Clouds FM ambacho hakuna ubishi kwamba, ni moja ya vituo bora
kabisa vya burudani nchini. Aliwakumbuka `vijana wa zamani’ kwa kuanzisha
kituo kingine cha redio, Choice FM pia cha jijini Dar es Salaam, lakini
kikiwa maalumu kwa muziki kwa watu maalumu, hasa wale wa kuanzia miaka ya
1950 hadi sasa.
Katika kituo hiki, ndipo utakapoweza kuusikia kwa kina muziki wa wakali
kuanzia akina Frank Sinatra, Billie Holiday, Bon Jovi, Prince na Celine
Dione hadi Heather Hedley, Norah Jones, Oliver Mtukudzi hadi muziki wa
kizazi kipya.
Ubunifu wake ulimfanya kuibuka na Coconut FM, kituo cha redio
kinachotamba katika visiwa vya Zanzibar tangu mwaka 2001.
Baada ya kukamilisha ngwe ya kwanza ya mipango yake mingi, angalau sasa
Kusaga anaweza kupumua na kusema kwa asilimia kubwa, lengo la kuwapatia
vijana sehemu ya kutolea sauti zao na kutangaza kazi zao za kisanii
limefikiwa ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za ajira kwa zaidi ya vijana
100.
“Wasanii wengi maarufu na watangazaji wenye vipaji wamefahamika kupitia
redio Clouds akiwamo Amina Chifupa (sasa marehemu)…ni wazi kuwa Clouds
inaibua vipaji vya vijana,” anasema Mkurugenzi huyo kijana ambaye kiumri
ndiyo kwanza yuko mwanzoni mwa miaka ya 40's.
Mafanikio ya jumla katika vituo vya redio yalimsukuma kuanzisha kituo
chake cha televisheni ambacho tayari kimeshaanza kuwa gumzo jijini Dar es
Salaam, Clouds TV.
Na uthibitisho wa mafanikio hayo ni tuzo ya SuperBrand ya hivi karibuni
ikitambua mchango wa kituo hicho kilichopewa hadhi ya ubora miongoni vya
vituo vya redio za burudani nchini.
Anafahamisha kuwa mafanikio yake yanatokana na dhamira aliyojiwekea tangu
akiwa na umri wa miaka 17 kuwa atatumia kipaji na nguvu zake kutatua
matatizo ya kijamii kwa kuwasaidia vijana hususani wanaojihusisha na
muziki.
“Namshukuru Mungu baba yangu aliniunga mkono kwani asilimia kubwa ya
vijana wanaojihusisha na muziki hupigwa vita kuanzia ngazi ya
familia…hivyo naahidi kuendelea kuwasaidia vijana wanaoibukia katika
muziki,” anaeleza.
Akielezea uzoefu wake katika masuala ya muziki, Kusaga anasema ameanza kazi
ya U-dj angali mtoto.
Kwa kuwa baba yake alikuwa mpenzi wa muziki nyumbani kwao kulikuwa na
vifaa vingi vya muziki hivyo akiwa shule ya msingi alitumia vifaa hivyo
kuchagua nyimbo mbalimbali kisha kuwaalika rafiki zake kucheza disko.
“Baba yangu alikuwa mpenzi wa muziki hivyo nilipokuwa mdogo ilikuwa
nawaalika rafiki zangu kuja nyumbani kucheza muziki ambapo mimi nilikuwa
DJ kwa kuchagua nyimbo na kuzipiga,” anasema Kusaga aliyeongeza kwamba,
baba yake ambaye kwa sasa ni marehemu, alimnunulia vifaa vya muziki vya
kisasa hivyo kupata uwezo wa kupiga muziki ambao mashabiki walisema
unapasua mawingu, hivyo kuzaliwa jina la `Clouds’, yaani `Mawingu’.
Lakini kabla ya kujikita katika biashara hasa ya burudani, alipata fursa
ya kusomea ufundi umeme katika kilichokuwa Chuo cha Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) mjini Morogoro ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha
Waislamu.
“Nilisoma ili niweze kutengeneza vifaa vya umeme katika redio na mitambo
ya muziki….pia nimesomea masuala ya ujasiriamali na kozi fupifupi za
uongozi na utangazaji,” anasema Kusaga, mume wa Juhayna Ajmy ambaye pia
ni mkurugenzi wa kitengo cha burudani cha Clouds na ofisa mwandamizi wa
Primetime Promotions. Amebahatika kuzaa naye watoto wawili, Natalia na
Zalex.
Pamoja na kazi nyingi, Kusaga hutenga muda wa kujumuika na familia yake,
ana anapopata nafasi anapenda kuogelea. Pia anapenda kusafiri na
kujifunza mambo mbalimbali katika nchi za wengine hususani matumizi ya
teknolojia mpya.
Ana ushauri gani wa vijana katika kutimiza ndoto zao za maisha? Anasema:
“Vijana wajiingize katika shughuli wanazozipenda badala ya kufuata
mkumbo. Na kwa wasanii chipukizi wajenge tabia ya kujiheshimu, kufanya
kazi kwa bidii na kuweka malengo katika bora katika maisha.
“Wasanii wanapaswa kuvaa vizuri, kuwa na tabia nzuri na kuweka malengo na
mipango endelevu katika maisha kwa kuzingatia kuwa ujana unapita,”
anasisitiza. Pia amewataka wasanii kujiendeleza kielimu, ikiwa ni pamoja
na kuhudhuria matamasha na maonyesho ya kimataifa ili kupanua wigo wa
kufikiri.
Kupitia kampuni yake ya Primetime, Kusaga akishirikiana na Mkurugenzi
mwenza, Ruge Mutahaba, wameweza kufanikisha ujio wa wasanii nyota wa
kimataifa nchini kwa udhamini wa makampuni mbalimbali, miongoni mwao
wakiwa Youssou Ndour, Angelique Kidjo, Fally Ipupa, Mbilia Bel, Fat Joe,
P Square, Shaggy, 50 Cent, Kevin Lyttle, Koffi Olomide, DNA, Jay Z na
mchumba wake Beyonce.
Pia wamo Ja Rule, Hugh Masekela, Mya, 2Face Idibia, Miriam Makeba, Wayne
Wonder, Sean Paul, Wenge BCBG na nyota wengine wengi wa nchi za Afrika
Mashariki na Kati.
Anamalizia kwa kuwashauri vijana wanaohisi wanaonewa au kudaiwa rushwa
ili nyimbo zao ziweze kupigwa katika kituo chake watoe taarifa kwa
uongozi wa juu.
Hata hivyo anasema redio inatoa kazi za wasanii kwa kuzingatia viwango
hivyo wasanii ambao hawajafikia viwango wanaimarishwa kwa kupitia
matamasha mbalimbali.
Huyo ndiye Joseph Alex Kusaga, `mtukutu’ aliyejipangia aina ya maisha
tangu akiwa mtoto, na leo hii ana kila sababu ya kujipongeza kwa kutimiza
ndoto yake ya kumiliki kituo cha redio.
|
No comments:
Post a Comment