MWENYEKITI wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi
amesema Watanzania wengi wanazidi kuwa masikini kwa sababu hawazitumii fursa za
utajiri uliopo nchini, hivyo kutaka vijana kuona kwa macho fursa hizo ili
waweze kujikwamua kutoka kwenye dimbwi hilo la umasikini.
Akizungumza wakati wa
kutoa zawadi kwa washindi watatu wa shindano la nini kifanyike kuzalisha ajira
nyingi hapa nchini aliloanzisha Mwenyekiti huyo wa IPP, Mengi alisema baada ya
Watanzania kupofushwa kuwa nchi yao ni masikini, wengi walibweteka na kushindwa
kuchangamkia fursa zilizopo hali ambayo imeifikisha nchi hapa ilipo.
Alisema jambo la msingi kwa vijana wa Tanzania ni kuibua
mawazo ya shughuli gani atafanya badala ya kukimbilia namna ya kupata mitaji,
kwani wengi ambao wamekimbilia kutafuta mitaji wamejikuta wanaipata mitaji
hiyo, lakini wakashindwa namna ya kuitumia.
Washindi katika shindano
hilo ambalo limeanzishwa na Mengi lijulikanalo kama Tweet Bora ni Lilian Wilson
wa Chuo Kikuu cha Ardhi aliyepata Sh milioni moja, Susan Senga ambaye ni mfanyabiashara
ndogo alipata Sh 500,000 na Ombeni Kaaya ambaye ni mjasiriamali kutoka Nzega,
Tabora aliyekabidhiwa Sh 300,000.
Katika maoni yao, Lilian
alipendekeza kuwa ili kuondoa tatizo la ajira wajasiriamali waliofanikiwa na
Serikali waanzishe mifuko ya kuwekeza mitaji kwenye biashara za vijana zenye
uwezekano wa kukua haraka badala ya kutegemea mikopo ya benki au taasisi za
fedha.
Susan Senga yeye alipendekeza kuanzishwe vipindi maalumu
kutoa elimu ya ujasiriamali ya kuwawezesha vijana kuwatoa katika fikra ya
kuishi kutegemea ajira ili kujiairi.
Kwa upande wake, Ombeni Kaaya katika maoni yake alisema
tafiti wanazofanya wanafunzi wa elimu ya juu mwaka wa mwisho zihusu jinsi
watakavyojiajiri katika fani zao kwani itasaidia wengi wajiajiri.
Naye Dk Donath Olomi wa
Taasisi ya Management and Entrepreneurship Development ambao ndio wanaoteua
washindi, alisema katika shindano la mwezi huu jumla ya maoni 979 yalipokewa na
watachagua washindi watatu kutoka katika maoni hayo
No comments:
Post a Comment